
Tatizo la Kondo la Nyuma (Placenta) Kuachia Kabla ya Mtoto Kuzaliwa (Placenta Abruption)
Tatizo hili linaweza kutokea ghafla wakati wa ujauzito. Inaweza kuwa hatari kwako na mtoto wako hivyo msaada wa haraka unahitajika. Kwa bahati nzuri sio tatizo linalowapata wajawazito wote.
Kondo la nyuma (placenta) inakua ndani ya mfuko wa uzazi ukiwa mjamzito. Kiungo hiki kinatumika kumlisha mtoto akiwa tumboni kwa mama yake kwa kutuma chakula virutubisho na hewa ya oksijeni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, na kutoa taka mwili zinazojijenga katika damu ya mtoto. Kondo la nyuma limejishikilia kwenye ukuta wa uterasi na mtoto wako amejishikilia kwenye kondo la nyuma kwa kutumia kiunga mwana (umbilical cord). Katika hali ya kawaida, kondo la nyuma hujitenga na ukuta wa mfuko wa uzazi mara baada ya mtoto kuzaliwa. Ukipata tatizo hili, kondo la nyuma hujitenga na ukuta wa mfuko wa uzazi kabla hata mtoto kuzaliwa (placenta abruption), ambapo husababisha mama kupoteza damu nyingi, kufariki kwa mtoto na hata mama mwenyewe.
Dalili na Ishara za Kondo la Nyuma Kuachia Kabla Mtoto Kuzaliwa (Placenta Abruption).
Tatizo hili linaathiri takribani asilimia moja ya wajawazito. Linatokea mda wowote baada ya wiki 20 za ujauzito, lakini pia linatokea sana katika kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito (third trimester).
Tatizo hili hutokea ghafla unaweza kuona damu ikitoka ukeni. Kiasi cha damu inayotoka ukeni kinatofautiana. Wakati mwingine kiasi kidogo cha damu hutoka ukeni kwasababu damu hunaswa ndani ya mfuko wa uzazi. Hivyo usidharau tatizo kwasababu kiasi cha damu kilichotoka ni kidogo, pata msaada wa haraka ikiwa dalili hiyo ya damu kutoka ukeni imeambatana na dalili hizi nyingine:
- Maumivu katika tumbo au mgongo
- Mibano na mikazo ya haraka au taratibu katika mfuko wa uzazi
- Matatizo katika mapigo ya moyo ya mtoto
Tatizo la kuachia kondo la nyuma linaweza kutokea kidogo kidogo “chronic abruption”. Unaweza shuhudia:
- Damu nyepesi kutoka na kuacha ukeni
- Kiwango kidogo cha “amniotic fluid”
- Mtoto aliye tumboni hakui haraka kama anavotakiwa.
Tatizo Hili la Kuachia Kondo la Nyuma Linasababishwa na Nini?
Wakati mwingi, madktari hawajui chanzo. Lakini unywaji wa pombe au matumizi ya madawa ya kulevya ukiwa mjamzito inaweza kuongeza hatari ya kupata tatizo hili. Vitu vingine vinavyochangia ni pamoja na:
- Ulipata tatizo hili katika mimba zilizopita. Kama tatizo hili lilishawahi kukupata hapo awali una nafasi ya takribani asilimia kumi tatizo hili kutokea tena katika ujauzito wa sasa.
- Uvutaji sigara. Utafiti mmoja ulionyesha wanawake waliokuwa wanavuta sigara kabla ya kushika ujauzito waliongeza nafasi ya kupata tatizo la kondo la nyuma kuachia kwa asilimia 40 kila mwaka waliovuta sigara.
- Matumizi ya kokeni au madawa mengine ya kulevya. Tatizo hili linatokea kwa asilimia 10 ya wanawake wanaotumia madawa haya katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito (third trimester).
- Shinikizo kubwa la damu kabla na baada ya kupata ujauzito, hakikisha mnalitafutia ufumbuzi tatizo hili wewe na mkunga wako ili liweze kudhibitiwa. Takribani ya nusu ya vifo vya watoto wachanga vinavyotokana na tatizo hili vinasababishwa na shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito.
- Matatizo ya kifuko cha maji yanayopatikana katika mfuko wa uzazi. Kifuko hichi cha maji kinatumika kumlinda mtoto ndani ya mfuko wa uzazi. Ikiwa kitu chochote kitapasua au kusababisha kuvuja kabla hujawa tayari kujifungua, nafasi ya kupata tatizo la kondo la nyuma kuachia inaongezeka.
- Kushika ujauzito ukiwa na umri mkubwa. Nafasi ya kupata tatizo hili huongezeka kama una umri wa miaka 35 au zaidi. Mara nyingi kama mama ana umri zaidi ya mika 40.
- Ukishika ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja. Wakati mwingine kujifungua mtoto wa kwanza kunafanya plasenta ijiachie kabla mtoto mwingine hajawa tayari kuzaliwa.
- Kuumia eneo la tumbo. Inaweza kutokea kama ulidondoka au kupata kipigo kikali tumboni. Inaweza kutokea kama ulihusika katika ajali ya gari, kumbuka kufunga mkanda wa gari kila mara.
Haiwezekani kuzuia tatizo la kondo la nyuma kuachia, lakini kuna vitu unaweza kuepuka kama vile tumbaku, pombe na madawa ya kulevya ili kupunguza nafasi ya kupata tatizo hili.
Mwambie mkunga au daktari wako anayesiamamia maendeleo ya ujauzito wako ikiwa ulipata tatizo hili katika mimba zako za awali. Watakuangalia kwa ukaribu zaidi. Watakushauri njia unazoweza kujikinga ili lisitoke tena.
Vipimo na Uchunguzi wa Tatizo la Kondo la Nyuma Kuachia.
Ikiwa unatoka damu ukeni au maumivu ya tumbo unahitaji kumuona daktari mara moja. Watakufanyia kipimo cha mwili na vipimo vya damu, pia watakufanya kipimo cha ultrasound kuona ndani ya mfuko wa uzazi (kipimo cha ultrasound hakionyeshi tatizo la kondo la nyuma kuachia).
Matibabu ya Tatizo la Kondo la Nyuma Kuachia.
Kondo la nyuma haliwezi kujifunga tena kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi, chaguo la matibabu linategemea na umri wa ujauzito wako, ukubwa wa tatizo na hali ya mama na mtoto.
Ikiwa una ujauzito chini ya wiki 34, utalazwa hospitali kwaajili ya kuangaliwa kwa ukaribu kama mapigo ya moyo ya mtoto ni kawaida na tatizo la kuachia kondo la nyuma sio kubwa. Ikiwa mtoto wako ataonekana kuendelea vizuri na damu ikacha kutoka unaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Ikiwa una ujauzito wa zaidi ya wiki 34, unaweza kujifungua kwa njia ya kawaida kama tatizo sio kubwa sana. Kama tatizo ni kubwa na limehatarisha afya yako na mtoto, upasuaji utahitajika kufanyika haraka. Pia unaweza kuhitaji kuongezewa damu.
Matatizo Yanayosababishwa na Tatizo la Kondo la Nyuma Kuachia.
Ikiwa sehemu ndogo ya kondo la nyuma itaachia, inaweza isisababishe matatizo mengi. Lakini kama sehemu kubwa au yote imeachia inaweza kusababisha athari kubwa kwako na mtoto wako. Kwa mjamzito inaweza kusababisha:
- Kupoteza damu nyingi inayoweza kusababisha mshtuko au kuhitaji kuongezewa damu
- Matatizo ya damu kuganda
- Figo au ogani nyingine kushindwa kufanya kazi
- Kifo- mama au mtoto.
Kwa mtoto matatizo yanayoweza kumpata ni kama:
- Mtoto kuzaliwa kabla ya mda (kabla ya wiki ya 37).
- Matatizo katika ukuaji wake. Watoto njiti wanaozaliwa kwasababu ya tatizo hili wanapatwa na matatizo mengi ya kiafya mwanzo na mwisho katika maisha yao.
- Mtoto kufariki akiwa tumboni baada ya angalau wiki ya 20 ya ujauzito.
IMEPITIWA: OKTOBA,2021.