Mtandao #1 kwa Afya ya Mama na Mtoto

Address:

P. O. Box 38995, Dar es Salaam, Tanzania

Kutoka Kwa Mimba Changa (Miscarriage)

Kutoka kwa mimba changa ni nini?

Miscarriage au kutoka kwa mimba changa ni kupoteza ujauzito kabla haujafikia wiki ya 20. Jina la kitaalamu kwa upotevu huu wa ujamzito mchanga ni “Spontaneous abortion” ikimaanisha “upotevu mimba wa ghafla”.

Zaidi ya asilimia 80 ya upotevu mimba changa hutokea katika miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito. Upotevu wa mimba ni vigumu kutokea baada ya wiki 20 za mwanzo za ujauzito kupita. Na kama ikitokea madaktari huita hali hii kama upotevu mimba uliochelewa “Late miscarriage”.

Dalili za upotevu mimba changa

Dalili za “miscarriage” ni pamoja na:

  • Kutoka kwa damu inayoanza kutoka kidogo kidogo na kuendelea mpaka kuanza kutoka kwa wingi
  • Maumivu makali ya tumbo la kukata (cramps)
  • Maumivu ya tumbo
  • Uchovu
  • Maumivu ya mgongo yanayoongezeka
  • Homa inayoambatana na dalili zozote kati ya hizo hapo juu
  • Kupungua uzito
  • Kutoka uchafu mweupe wenye upinki ukeni
  • Kukaza kwa misuli ya nyonga (contractions)
  • Kutoka kwa vinyama nyama kama damu iliyoganda kutoka ukeni
  • Dalili dhoofu za ujauzito

Kama una dalili kati ya hizo hapo juu ni vyema kuhudhuria kituo cha afya kwa ushauri Zaidi. Watakuambia kama ni dalili za dharura au kufanyiwa vipimo kuchunguza ujauzito wako kwa ujumla.

Nini husababisha upotevu wa mimba changa kutokea?

Mara kwa mara kutoka kwa mimba changa hutokea pale mtoto anaekua tumboni akiwa na matatizo ya kigenetiki. Matatizo haya hayana uhusiano na mama.

Matatizo mengine yanayoweza kusababisha uwezekano wa kutoka kwa mimba changa ni kama:

  • Maambukizi
  • Matatizo ya kiafya kwa mama kama ugonjwa wa kisukari au matatizo ya thairoidi
  • Matatizo ya mfumo wa homoni
  • Matatizo katika uitikiaji kinga mwili (Immune response)
  • Matatizo ya kimaumbile kwa mama
  • Matatizo katika umbo la mfuko wa kizazi
  • Uvutaji wa sigara
  • Unywaji wa pombe
  • Matumizi ya madawa ya kulevya
  • Kuwa kwenye uwepo wa ukaribu na mionzi au viambata sumu

Mwanamke anakuwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupoteza mimba ikiwa changa kama:

  1. Ana umri zaidi ya miaka 35
  2. Ana matatito mengine ya kiafya kama kisukari na matatizo ya kithairoidi
  3. Ameshawahi kupata kupoteza mimba changa mara tatu au zaidi

Udhoofu au kulegea kwa mlango wa mfuko wa uzazi (Cervical Insufficiency)

Kutoka kwa mimba ikiwa changa mara nyingine hutokea pale mama mjamzito anapokuwa na udhoofu au ulegevu wa mlango wa kizazi. Hii inamaanisha mlango wa kizazi hauwezi kuhimili ujauzito kikamilifu na hivyo kufunguka na ujauzito kutoka kabla ya muda wake. Mara nyingi aina hii ya upotevu wa ujauzito mchanga hutokea katika hatua ya pili ya ujauzito. Huwa kuna dalili chache sana kabla ya upotevu wa aina hii kutokea. Unaweza ukahisi mkandamizo wa ghafla, unaweza ukavunja chupa (maji mengi kutoka ukeni), na nyama nyama pamoja na kondo la nyuma la ujauzito kutoka ukeni bila ya kupata maumivu makali.

Madaktari kwenye nchi zilizoendelea hutibu aina hii ya upotevu mimba changa kwa kushona nyuzi kwenye mlango wa kizazi kwenye ujauzito wako utakaofuata. Hufanya hivi kwenye walau wiki ya 12 ya ujauzito. Nyuzi hizi zitasaidia kuufanya mlango wa kizazi uendelee kufungwa mpaka utakapokaribia kujifungua ndipo nyuzi hizi hutolewa na utajifungua kawaida.

Aina za kutoka kwa mimba changa

Kuna aina mbalimbali za upotevu mimba changa, kama:

Upotevu mimba changa hatarishi. Hii hutokea pale unapokuwa unatokwa na damu na kuna hali ya hatari kwa mama kupoteza ujauzito wake lakini mlango wa kizazi haujafunguka. Katika hali hii kama sababu za kutokwa kwa damu zitatatuliwa basi ujauzito huendelea bila matatizo.

Upotevu mimba changa usioepukika. Hapa mama mjamzito hutokwa na damu na pia anakuwa na maumivu ya tumbo mkazo (crampings), na pia mfuko wa kizazi umefunguka. Uwezekano wa kutoka kwa mimba changa kwenye hali hii ni wa hali ya juu sana.

Upotevu mimba changa usiokamilika. Baadhi ya nyama nyama kutoka kwa mtoto wako na sehemu ya kondo la nyuma na mfuko wa mimba vinatoka nje ya uke na baadhi vinabaki ndani ya uke.

Upotevu mimba changa uliokamilika. Ujauzito wote unatoka nje ya mwili wako. Kila kitu kinatoka, yaani, mtoto, mfuko wa mimba na kondo la nyuma. Aina hii mara nyingi hutokea kabla ya wiki ya 12 ya ujauzito kufika.

Upotevu mimba ulionusurika. Aina hii inahusisha kifo cha kiini cha mimba lakini nyama nyama za ujauzito husika zinabaki kwenye mfuko wa uzazi bila kutoka nje.

Upotevu mimba changa unaojirudia rudia. Aina hii inatambulika pale unapopoteza mimba zaidi ya tatu mfululizo ambazo hazikufikia umri wa zaidi ya wiki 12. Aina hii ya upotevu mimba changa hutokea kwa asilimia moja tu (1%) ya wenza wanaojaribu kupata mtoto.

Daktari atatambuaje kwamba una tatizo la upotevu mimba changa?

Kuhakikisha kwamba umepata upotevu mimba changa, daktari wako atafanya yafuatayo:

  • Uchunguzi wa mlango wako wa kizazi kuangalia kama umefunguka
  • Kipimo cha “ultrasound” Hapa atajaribu kuangalia maendeleo ya mtoto tumboni na kutafuta mapigo ya moyo ya mtoto. Kama itashindikana kupata jibu la moja kwa moja kipimo hiki kinaweza kurudiwa baada ya wiki moja.
  • Vipimo vya damu. Hapa daktari ataangalia uwepo wa homoni za ujauzito kwenye damu yako na kulinganisha kiwango cha homoni hizi na vipimo vilivyofanywa hapo awali. Pia ataangalia wingi wa damu kama umekuwa ukitokwa na damu nyingi ukeni.
  • Vipimo vya vinyama vinyama vilivyotoka ukeni pia huweza kufanyika kama vilikuwa vinatoka. Hii husaidia kuwa na uhakika kwamba umepata upotevu mimba changa na pia kuweza kutambua kama kuna matatizo mengine yanayosababisha kupatwa na tatizo hili.
  • Kipimo cha kromosomu (chromosome test). Kipimo hiki kinaweza kufanyika kama wewe na mwenza wako mmepoteza zaidi ya mimba changa mbili mfululizo. Daktari atachunguza kama mfumo wenu wa genetiki ndio unaosababisha upotevu huu.

Matibabu ya upotevu mimba changa

Asilimia 85% ya wanawake wanaopata upotevu mimba changa hufanikiwa kupata ujauzito salama na kujifungua salama baadae. Kupata upotevu mimba changa haimaanishi una tatizo la uwezo wa kupata watoto. Kwa upande mwingine, karibia asilimia 1 mpaka 2 ya wanawake hupata upotevu mimba changa unaojirudia rudia. Yani mara tatu au zaidi. Baadhi ya watafiti wanaihusisha hali hii na magonjwa ya ukinzani wa kinga mwili binafsi (autoimmune diseases)

Kama umepata upotevu mimba changa mara mbili mfululizo, ni vyema kuacha kujaribu kupata ujauzito, tumia uzazi wa mpango na wasiliana na mtaalamu wa afya ili waweze kutambua sababu ya upotevu wako wa mimba changa mfululizo.

Kama upotevu wako wa mimba changa ni uliokamilika na mfuko wa uzazi ni mtupu, inawezekana hautahitaji matibabu zaidi.

Wakati mwingine sio tishu zote na nyama nyama hutoka nje ya mfuko wa uzazi. Kama hili litatokea, daktari wako atafanya “Dilation and Curretage”. Haya ni matibabu ambayo itambidi daktari aupanue mlango wa uzazi na kutoa kila kitu kilichabaki kwenye mfuko wa uzazi kwa umakini. Pia kuna madawa ambayo ukitumia husaidia kutoa tishu zilizobaki kwenye mwili ziweze kutoka nje.

Baada ya utokaji wa damu kuisha unaweza ukaendelea na shughuli zako za kila siku. Kama mlango wako wa uzazi umefunguka lakini ujauzito bado upo salama daktari wako ataweza kufunga mlango wa kizazi kwa kuushona ili kuepusha ujauzito kutoka mpaka pale wakati wa kujifungua utakapofika.

Kama kundi la damu yako ni lile lenye Rh hasi (Rh-), daktari wako anaweza akakupa chembechembe tiba za damu ziitwazo (Rh Immune Globulin). Hizi husaidia kuepusha wewe kutengeneza kinga mwili (antibodies) ambazo zinaweza zikamdhuru mwanao au mimba zijazo.

Unaweza ukafanyiwa vipimo vya damu, vipimo vya genetiki au madawa kama umeshapata upotevu mimba changa mara mbili mfululizo. Kuweza kuhakikisha kwamba una upotevu mimba changa mfululizo (recurrent miscarriages) daktari wako atafanya vipimo vifuatavyo:

  • “Ultrasound” ya nyonga
  • Hysterosalpingogram (Hii ni X-ray ya mfuko wa uzazi na mirija ya uzazi kwa pamoja)
  • Hysteroscopy (Daktari wako atatumia mrija mrefu mwembaba wenye mwanga na kamera kuingia kwenye mfuko wako wa uzazi kuweza kuona kama una matatizo yoyote)

Dalili mbalimbali baada ya kupata upotevu mimba changa

Kutoka kwa damu na hali ya kujisikia vibaya ni dalili mojawapo baada ya kupata upotevu mimba changa. Kama utakuwa na kutoka kwa damu nyingi ikiambatana na homa, mwili kutetemeka na maumivu makali, hudhuria kituo cha afya haraka kwani hizi ni dalili za maambukizi.

Pamoja na dalili za kimwili unaweza pia ukawa unajihisi kuwa na hisia za huzuni, kujilaumu na pia kuwa na wasiwasi kuhusu mimba zitakazofuata. Unachojisikia ni kawaida na ni vyema kupitia hatua hii ya huzuni kuliko kuipotezea mbali na kuiacha ikusononeshe ndani kwa ndani.

Kama unaweza na hautajali, ni vyema kuliongelea swala hili na watu wako wa karibu kama mwenza wako, rafiki au mwanafamilia uliyemzoea. Vikundi vya wamama waliopoteza mimba kwenye jamii vinaweza kuwa na manufaa makubwa kwako na kwa mwenza wako. Pia muulize daktari wako kama kuna taarifa au ushauri wa ziada ambao anaweza kukupatia. Kumbuka kila mtu anapona na kuhuzunika na kurudia hali yake ya kawaida tofauti. Hivyo usikate tamaa.

Kupata mimba tena baada ya upotevu wa mimba changa

Unaweza ukapata ujauzito tena baada ya upotevu wa mimba changa. Zaidi ya 85% ya wanawake waliojaribu mara moja baada ya kupoteza mimba changa walipata ujauzito na kuendelea na kuja kujifungua salama. Kuwa na upotevu wa mimba changa haimaanishi kwamba una tatizo kwenye uwezo wako wa kupata mtoto. Hivyo hivyo asilimia 1 mpaka 2 ya wanawake wanaweza wakapata upotevu mimba changa unaojirudia rudia (mara tatu au zaidi).

Kama umepata upotevu mimba changa mara mbili mfululizo, ni vyema kuacha kujaribu kupata ujauzito, tumia uzazi wa mpango na wasiliana na mtaalamu wa afya ili waweze kutambua sababu ya upotevu wako wa mimba changa mfululizo.

Ni wakati gani ujaribu kupata ujauzito tena baada ya kupoteza mimba changa

Ni vyema kufanya mazungumzo haya na daktari wako. Wataalamu wengine wa afya wanasema ni vyema kusubiria kwa muda fulani kabla ya kupata ujauzito mwingine. Muda kati ya mzungumko mmoja wa hedhi mpaka miezi mitatu kabla ya kufikiri kujaribu tena kupata ujauzito. Kuzuia upotevu mwingine wa mimba changa daktari wako anaweza kukupa matibabu kutumia “Progesterone”, homoni inayosaidia kiini mimba kujishika kwenye mfuko wa uzazi na kusaidia maendeleo yake kwenye hatua za mwanzo za ujauzito.

Kuchukua muda kupona kimwili na kiakili ni muhimu pia baada ya kupoteza mimba changa. Ni vyema kutokujilaumu na kujiona mwenye makosa. Hakikisha unapata msaada wa kimawazo na ushauri kujitayarisha na kuwa tayari pale utakapoweza kujaribu tena.

Je, utazuiaje kutokea kwa upotevu mimba changa?

Upotevu mimba changa mara nyingi hutokea kwa sababu kuna tatizo kwenye ujauzito husika. Huwezi kuzuia hili. Kama daktari wako atakupima na kuona tatizo, aina mbalimbali za matibabu zinapatikana.

Kama una ugonjwa, kuutibu ugonjwa husika kutaongeza uwezekano wa kupata ujauzito ulio salama na kujifungua bila matatizo. Njia bora unayoweza kuchukua mwenyewe ni kuhakikisha unakuwa mwenye afya kadiri uwezavyo kabla ya kujaribu kupata ujauzito:

  • Fanya mazoezi ya mara kwa mara
  • Kula mlo kamili na wenye afya
  • Zingatia kuwa kwenye uzito wako kiafya
  • Epuka maambukizi
  • Usivute, kunywa pombe au kutumia madawa ya kulevya
  • Punguza utumiaji mkubwa wa “caffeine” kama kahawa.

IMEPITIWA: MARCH 2021

Matumizi ya Dawa Kipindi cha Ujauzito

Mara kwa mara wanawake wengi hugundua kuwa ni wajawazito baada ya kukosa hedhi. Hivyo ni vyema kutambua madhara ya madawa mbali mbali hata kabla hujafikiria kuwa mjamzito ili ujue nini cha kuepuka.

Dawa nyingi hazijafanyiwa majaribio kama ni salama kwa ujauzito. Unachoweza kufanya kuepuka matatizo ni kuamua kutotumia dawa yoyote katika ujauzito wako labda tu uwe umeshauriwa na daktari.

Dawa mbali mbali zinaweza zikaathiri ukuaji wa mtoto wako kwa njia nyingi, ikiwemo:

  1. Kubadilisha mazingira ya mji wa mimba hivyo kusababisa uhaba wa mahitaji muhimu kwa mtoto
  2. Kubadilika kwa uwiano wa ukuaji sahihi wa mtoto hivyo kusababisha mtoto kuzaliwa njiti
  3. Kusababisha kuzaliwa na matatizo au mimba kutoka
  4. Kusababisha matatizo ya kupumua baada ya mtoto kuzaliwa

Kama unatumia dawa za aina yoyote ile na umegundua kuwa ni mjamzito ni vyema kuwasiliana na daktari wako mara moja kabla hujaacha kuzitumia kwani maisha yako yanaweza yakawa yanategemea dawa hizi. Daktari wako ataweza kukushauri kuhusu dawa unazotumia kama ni salama au la kwenye ujauzuto na kukubadilishia kadiri itakavyoonekana ni sawa.

Ni vyema pia kuwa makini na dawa zinazoitwa za asili. Kwa sababu tu zimeandikwa ni dawa za asili haimaanishi hazina uwezo wa kuleta shida kwenye ujauzito wako. Dawa nyingi za asili pia zina uwezo wa kuleta matatizo kipindi cha ujauzito hivyo ni vyema kutokutumia dawa za asili ukiwa mjamzito.

Dawa yoyote ile ambayo utaitumia mwilini kwako kipindi cha ujauzito ni vyema iwe imetolewa na daktari wako anaetambua kwamba wewe ni mjamzito. Baadhi ya wanawake hununua dawa kwenye maduka ya dawa baridi kama Paracetamol pale wanapohisi maumivu. Ni vyema pia kupata ushauri wa daktari kwani kuna baadhi ya dawa za maumivu unaweza ukawa unahisi ni salama (kwani si za maumivu tuu), kumbe zinaweza kuleta shida kwako au kwa mtoto wako tumboni.

Kuweza kuepuka mahitaji ya kutumia dawa kipindi cha ujauzito, kula mlo bora, kunywamaji ya kutosha, fanya mazoezi na pia jifunze kupumzika. Msongo wa mawazo unaweza kusababisha kila maumivu kuwa makali zaidi. Maswali yoyote kuhusu dawa ni vyema ukashirikiana na daktari wako kwani yeye ndiye mwenye uwezo na taarifa sahihi kuhusu usalama wa dawa husika na usalama wako na mtoto wako.

Mambo Yanayotakiwa Kufanyika Unapohudhuria Kliniki za Ujauzito

Nani anayetoa huduma?

Kama una afya na unategemea kuwa na ujauzito salama katika miadi yako ya kliniki utahudumiwa na mkunga au manesi maalumu wa afya ya uzazi. Ikiwa una historia ya matatizo ya kiafya, kama shinikizo la damu utapelekwa kwa mtaalamu wa mambo ya uzazi na wajawazito.

Lini nitakua na miadi yangu ya kwanza?

Muda wa miadi yako ya kwanza ya kliniki inategemea na mahali unapoishi. Mara mkunga wako au mshwauri wako wa afya amejua una mimba unaweza kuonana nae mara moja kabla ya miadi mikuu ambayo inaanza wiki ya 10. Katika miadi hii ya kwanza utafahamu kwanini unahitaji foloki asidi na utapewa taarifa muhimu kuhusu kula kwa afya.

 

Maswali nitakayoulizwa na mkunga wangu?

Jiandae kwa maswali mengi na fomu ya kujaza. Mkunga wako anataka kupata ujuzi wa afay yako, ya mpenzi wako na historia ya matibabu ya familia zote mbili.

Baadhi ya vitu utakavyoulizwa ni kama:

  • Tarehe yaa mwisho ya hedhi yako,itamsaidia kujua lini untarajia kujifungua.
  • Kama mimba ilishawahi haribika, kutoa au kama una mtoto,itamsaidia mkunga kujua aina gani ya huduma unahitaji kupewa kipindi chote cha ujauzito.
  • Magonjwa ya kurithi katika familia zenu zote mbili, kama vile kisukari,magonjwa ya moyo, magonjwa ya akili na kansa ya damu. Magonjwa haya yanaweza kurithiwa na kuleta shida wakati wa ujauzito hivyo kuwa muwazi kwa mkunga wako.

Kama una miaka chini ya 25,mkunga atafanya viimo vya ugojwa wa kuambukiza wa klamidia.

  • Kazi yako, kama umeajiriwa na aina ya kazi kwasababu baadhi ya kazi zinahatrisha ujauzito.
  • Maisha yako ya kila siku, mkunga atakuuliza kama unavuta sigara na kunywa pombe, maana yote haya yanaweza athiri afaya ya mtoto.
  • Wapi ungependelea kujifungulia mtoto wako.
  • Faida na haki za wamama wajawazito.
  • Kama unategemea kunyonyesha.

Mkunga wako atatumia taarifa uliyompatia kuamua kama unahitaji huduma ya zaidi kutoka kwa mtaalamu wa afya ya uzazi au la. Pia atakushauri:

  • Kufanya mazoezi wakati wa ujauzito hasa mazoezi ya sakafu ya nyonga
  • Kutumia virutubisho kama foliki aside na vitamin D
  • Kula kwa afya.

Vipimo nitakavyofanyiwa ni kama ifuatavyo:

Vipimo vya damu

Kipimo cha damu kitachukuliwa na kuimwa maabara ilikuangalia viwango vya haemoglobini, kundi la damu na kama damu yako ina wadudu hatari

Screening tests (kipimo cha uchunguzi)
Damu yako itachukuliwa ili kuchunguzwa kama mwanao ana hatari za  kuwa na ugonjwa wa akili (Down’s syndrome) au  tatizo la maumbile yake .

Damu yako itatumika kuchunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi, kaswende,kisonono na homa ya ini.

Kipimo cha mkojo

mkunga atakupa chupa kwaajili ya kuweka mkojo, na kuongeza kemikali kuangalia kama mkojo wako una protini. Katika siku za kwanza za ujauzito, protini katika mkojo wako ni dalili ya matatizo, yakiwepo:

  • UTI
  • Shida ya kibofu
  • Shinikizo kubwa la damu
  • Kisukari

Protini katika mkojo siku za mwisho za ujauzito wako zinaonyesha dalili za kifafa cha mimba. Protini katika mkojo wako mara kwa mara ina maanisha uchafu kutoka ukeni umeingia kwenye mkojo.

Kipimo cha shinikizo la damu
mkunga wako atakupima shinikizo la damu na kuandika kwenye kadi yako ya ujauzito. Shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito ni tahadhari za awali za dalili ya kifafa cha mimba.

Kipimo cha Ultrasound scan

Ni muhimu kujua mtoto wako anaendeleaje na jinsia yake pale mda utakapofika kama utapenda kujua.

Mara ngapi nitakua na miadi ya kliniki?

Hii inategemea na mahali unapoishi na kama mimba yako ni salama. Baada ya miadi yako ya kwanza ndani ya wiki ya 10, miadi mingine ifanyike:

  • Wiki ya 16
  • Wiki ya 25
  • Wiki ya 28
  • Wiki ya 31
  • Wiki ya 34
  • Wiki ya 36
  • Wiki ya 38
  • Wiki ya 40
  • Wikiya 41, kama mtoto hajazaliwa bado.

Utapewa kipeperushi kinachotoa habari kuhusu nini utegeme na lini kwenye miadi yako. Unaweza kujadiliana na mkunga wako ratiba  hii.

Kama huu ni ujauzito wako wa pili, itakubidi uwe na miadi saba tu,ikiwa mimba yako haina matatizo,miadi hiyo ni katika wiki ya:

  • Wiki ya 16
  • Wiki ya 28
  • Wiki ya 34
  • Wiki ya 36
  • Wiki ya 38
  • Wiki ya 41 kama mtoto hajazaliwa bado.

Ikiwa una wasiwasi na huwezi kusubiria mpaka miadi yako iliyopangwa, wasiliana na mkunga wako upate kuonana nae mapema. Matatizo ya kiafya na matatizo yaliyosababishwa na ujauzito yanasababisha afya ya mama mjamzito iangaliwe kwa ukaribu zaidi na wataalamu wa mambo ya uzazi. Mda mwingi katika miadi hii utaonana na daktari badala ya mkunga, na unaweza kufanyiwa uchunguzi sana kuliko wanawake wajawauzito wengine.

Tatizo mwishoni mwa ujauzito inaweza sababishwa na kupanda kwa shinikizo la damu au chupa ya uchungu kupasuka kabla ya uchungu kuanza hivyo utapelekwa kwenye wodi utakayoangaliwa kwa umakini zaidi.

Maambukizi Kipindi cha Ujauzito

Wakati wa ujauzito,mtoto wako analindwa na magonjwa mengi, kama mafua na chango. Lakini baadhi ya maambukizi haya yanaweza kuwa hatari kwa ujauzito wako, mtoto wako, au wote. Jedwali lifuatalo linaonyesha baadhi ya maambukizi ambayo yanaweza kuwa hatari wakati wa ujauzito.Ni vizuri kuzijua dalili na nini cha kufanya ili kuwa katika afya nzuri wakati wa ujauzito wako. Hatua rahisi kama kusafisha mikono, kufanya ngono salama, na kuepuka baadhi ya vyakula, kutasaidia kuepuka baadhi ya maambukizi.

 

Maambukizi wakati wa ujauzito
Maambukizi Dalili Kinga na tiba
Maambukizi ya bakteria ukeni-Bacterial vaginosis (BV)

Maambukizi ya ukeni yanayosababishwa na ukuaji uliopitiliza wa bakteria ambao kwa kawaida wanapatikana ukeni.

BV inapelekea mama kujifungua mtoto njiti na mtoto mwenye uzito pungufu.

 

  • Kutoka uchafu ukeni wenye rangi ya kahawia au nyeupe, na wenye  harufu.
  • Maumivu ya kuungua au kuwashwa wakati wa kukojoa.
  • Baadhi ya wanawake hawana dalili zozote.
 Maambukizi haya hayaambukizwi kwa njia ya ngono, japo yanahusishwa na kuwa na mwenzi wa ngono zaidi ya mmoja.

Wanawake wenye dalili za maambukizi haya lazima wapimwe.

Antibaotiki zinatumika kutibu maambukizi haya.

Cytomegalovirus (CMV)

Hiki ni kirusi cha kawaida kinachosababisha ugonjwa kwa watoto wachanga ambao mama zao walikua na maambukizi haya wakati wa ujauzito. Maambukizi ya ugonjwa huu kwa watoto wachanga yanasababisha ukosefu wa kusikia vizuri(ukiziwi), upofu na ulemavu mwingine.

  • Magonjwa madogo madogo yanayojumuisha homa,kuvimba tezi na uchovu.
  • Baadhi ya wanawake hawana dalili.
Usafi bora ni njia nzuri ya kuepuka kupata maambukizi haya.

Hakuna tiba maalum iliyopo kwa sasa. Wataalamu wanatafuta dawa za kudhibiti virusi kwa watoto wachanga. Pia wataalamu wanatengeneza chanjo ya maambukizi haya.

Group B strep (GBS)

Maambukizi haya yanasababishwa na bakteria anayeshambulia watoto wachanga,mama wajawazito, wazee na watu wazima wenye kisukari.

Bakteria wanapatikana ukeni na kwenye mkundu (rectum) wa wanawake wenye afya. Moja kati ya wanawake wanne anaweza kuwa na maambukizi.

Kwa kawaida GBS si hatari  kwa mama mjamzito ila ni mbaya kwa mtoto wako ikiwa ataambukizwa kutoka kwako wakati wa kujifungua.

  • Hakuna dalili.
Unaweza kuepuka kumuambukiza mtoto kwa kuhakikisha kupima wiki 35 mpaka 37 ya ujauzito. Kipimo kinafanyika kwa urahisi sana, kipimo maalum kinatumika kufuta ukeni na kwenye mkundu(rectum) ili kuchukua sampuli ya kupimwa. Kumbuka kipimo hichi hakiumi kabisa.

Ikiwa una maambukizi haya, antibaiotiki utakazopewa wakati wa kujifungua zitasaidia kumlinda mtoto na maambukizi. Hakikisha unawapa taarifa wakunga wako kwamba una maambukizi haya.

Ugonjwa wa homa ya ini B

Ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya hepatitis B vinavyoathiri ini na kuambukizwa kwa mtoto wakati wa kuzaliwa. Mtoto mchanga anayeambukizwa wakati wa kuzaliwa ana nafasi ya asilimia 90 ya  kupata maambukizi maisha yake yote. Hali hii husababisha uharibifu wa ini na kansa ya ini. Chanjo inayotolewa inaweza kumkinga mtoto mchanga. Ila 1 kati ya watoto 5  wachanga wanaozaliwa na wamama wenye maambukiz haya wanondoka hospitali bila chanjo

Dalili zinaweza zisionekane au kuonekana. Dalili zinazoonekana ni kama:

  • Kichefuchefu, kutapika, na kuharisha.
  • Mkojo mweusi na kinyesi cha rangi ya udongo udongo
  • Macho kuwa meupe au ngozi kuonekana ya njano.
Vipimo vya maabara vinaweza kugundua kama mama ana maambukizi ya homa ya ini.

Unaweza kumkinga mtoto maisha yake yote na chanjo ya homa ya ini inayotolewa mara tatu kwa kufuatana;

  • Dozi ya kwanza ya chanjo ya homa ya ini pamoja na sindano moja anayopewa mtoto wakati wa kuzaliwa.
  • Dozi ya pili ya chanjo ya homa ya ini inatolewa mtoto akiwa na mwezi au miezi 2.
  • Dozi ya tato ya chanjo ya inatolewa mtoto akiwa na miezi 6(sio kabla ya wiki 24).
Homa ya mafua

Mafua ni maambukizii ya kawaida yanayosababishwa na kirusi, yanaweza kusababisha ugonjwa mbaya kwa wanawake wajawazito kuliko wanawake ambao si wajawazito. Mwanamke aliye na ugonjwa huu ana nafasi kubwa ya kupata  matatizo makubwa na kwa mtoto ambaye atazaliwa kabla ya siku zake.

  • Homa (mara nyingine)
  • Kukohoa
  • Kuvimba tezi
  • Kubana kwa pua kwasababu ya kamasi.
  • Maumivu ya misuli na mwili.
  • Kuumwa kichwa
  • Kusikia uvivu
  • Kutapika na kuharisha(wakati mwingine)
Kupata sindano za mafua ni hatua ya kwanza na muhimu ya kujikinga na mafua. Sindano za mafua zinapatiwa wakati wa ujauzito ni salama na humkinga mama na mtoto (mpaka miezi 6), (chanjo ya kupuliza puani asipewe mama mjamzito).

Ikiwa unahisi kupata mafua wasiliana na daktari wako atakuagiza dawa za kutibu mafua.

 

Listeriosis( Ugonjwa wa Listeria)

Maambukizi yanayosababishwa na bakteria hatari aitwaye listeria. Anapatikana kwenye vyakula vilivyogandishwa na tayari kwa kuliwa.Maambukizi haya yanaweza sababisha kujifungua mapema kabla ya siku zako au kuharibika mimba.

  • Homa, misuli kuuma, kusikia baridi
  • Mara nyingine kuharisha au kusikia kichefuchefu
  • Hali ikiendelea, kichwa kinauma sana na shingo kukakamaa.
Epuka vyakula vya kuagizwa kutoka nchi nyingine.

Antibaiotiki zinatumika pia kutibu maambukizi haya.

Parvovirus B19 (fifth disease)

Wanawake wengi walio na maambukizi haya hawana tatizo kubwa sana. Lakini kuna nafasi chache ya kirusi kuambukiza kitoto kichanga tumboni. Hali hii inaongeza hatari ya mimba kuharibika ndani ya wiki 20 za kwanza za mimba.

Maambukizi haya pia yanaweza sababisha anemia (upungufu wa damu) kali kwa wanawake wenye tatizo la chembe nyekundu za damu kama ugonjwa wa selimundu(sickle cell) na matatizo ya mfumo wa kinga.

  • Homa ya chini
  • Uchovu
  • Upele juu ya uso, shingoni, na miguuni.
  • Maumivu na kuvimba viungo.
Hakuna matibabu maalum, isipokuwa kupewa damu hasa kwa wenye matatizo ya mfumo wa kinga au chembe nyekundu za damu. Hakuna chanjo inayoweza kukinga maambukizi haya ya virusi.
Maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STI)

Maambukizi ambayo yamepatikana kwa njia ya kujamiiana. Magonjwa mengi ya zinaa yanaweza kuambukizwa kwa mtoto tumboni au wakati wa kuzaliwa. Madhara mengine ni pamoja na mtoto kuzaliwa akiwa amefariki, uzito duni kwa mtoto, na maambukizi ya kuhatarisha maisha. Magonjwa ya zinaa pia yanaweza kusababisha chupa ya maji ya uchungu ya mwanamke kuvunjika mapema au kupata uchungu wa kuzaa mapema.

  • Dalili zinategemea na aina ya maambukizi ya ugonjwa wa zinaa. Mara nyingi mwanamke hana dalili,ndo maana uchunguzi wa kina wa magonjwa ya zinaa wakati wa ujauzito ni jambo muhimu sana.
Magonjwa ya zinaa yanaweza kukingwa kwa kufanya ngono salama. Mwanamke anaweza kumkinga mwanae na magonjwa ya ngono kwa kufanya uchunguzi wa kina mwanzoni mwa ujauzito.

Matibabu yanatofautiana kulingana na aina ya maambukizi. Maambukizi mengi ya zinaa yanatibika kwa urahisi na antibaiotiki.

Toxoplasmosis

Maambukizi haya yanasababishwa na vimelea vinavyopatikana kwenye kinyesi cha paka,udongo,na nyama mbichi au isiyopikwa vizuri. Maambukizi haya yakimfikia mtoto mdogo tumboni yanasababisha upofu, ukiziwi au matatizo ya akili.

  • Mafua kwa mbali au hakuna dalili kabisa.
Unaweza punguza hatari ya kuambukizwa kwa:

  • Osha mikono yako na sabuni baada ya kushika udongo au nyama mbichi.
  • Osha nafaka, matunda na mbogamboga vizuri kabla ya kula.
  • Pika nyama vizuri mpaka iive.
  • Osha vyombo vyako vya kupika na maji ya moto na sabuni.

 

Dawa zinatumika kumtibu mama mjamzito na wakati mwingine mtoto anatibiwa na dawa baada ya kuzaliwa.

Urinary tract infection (UTI)

Maambukizi ya bakteria katika mfumo wa mkojo. Maambukizi haya yasiotibiwa yanaweza kusambaa mpaka kwenye figo na kusababisha uchungu mapema kabla ya mda wa kujifungua.

  • Maumivu au kuungua wakati unakojoa.
  • Kukojoa mara kwa mara.
  • Maumivu ya nyonga, mgongo, tumbo, au upande.
  • Kutetemeka ,kusikia baridi,homa, kutokwa jasho.
UTIs  inatibika na antibaiotiki
 Yeast infection

Maambukizi yanayosababishwa na ukuaji wa kasi wa bakteria zinazopatikana ukeni. Maambukizi haya ni ya kawaida wakati wa ujauzito kuliko wakati mwingine wa maisha ya mwanamke. Maambukizi haya si hatari kwa afya ya mtoto wako. Lakini unaweza kuwa na wasiwasi na ugumu wa  kutibu wakati wa ujauzito. 

  • Kuwashwa kulikopitiliza maeneo ya ukeni
  • Kuungua,uwekundu na kuvimba uke na vulva
  • Maumivu wakati wa kukojoa au kufanya tendo la ndoa
  • Kutokwa na uchafu ukeni ulio mzito na mweupe kama jibini na wenye harufu mbaya.
Cream maalamu na vifaa maalumu vinatumika kutibu maambukizi haya.

 

Kujifungua kwa Msaada wa Vifaa Maalumu

Wakati mwingine inaweza ikashindikana kwa mwanamke kumsukuma mtoto wake atoke, anaweza kuwa kwenye madawa au mwenye uchovu mwingi. Kunaweza kukawa na matatizo yanayosababisha anashindwa kumsukuma mtoto, au dharura imetokea na inalazimu kujifungua kufanikiwe kwa haraka.

Chuma za kujifungulia (Forceps)           

Forceps (chuma za kujifungulia) zinatumiaka kushikilia na kuvuta kichwa cha mtoto kilichokwama ndani ya njia ya kujifungulia. Daktari wako anaweza akapasua kidogo uke wako kuongeza njia ya forceps kuweza kupita na baadae kichwa cha mtoto wako. Wakati wa mkazo wa misuli ya mfuko wako wa uzazi ukiwa unasukuma, daktari atavuta taratibu kwa msaada wa forceps. Kwa kawaida kama majaribio matatu ya kumtoa mtoto yatashindikana utahitajika kufanyiwa upasuaji.

 Kifaa utupu cha kuvutia (Ventouse/Vacuum extractor)

Njia hii inatumia kifaa kinachotumia nguvu ya utupu (vacuum). Kikombe chenye utupu kitawekwa juu ya kichwa cha mtoto wako na kuunganishwa kwenye pampu. Baada ya kufanikiwa kukikamata kichwa vizuri kwa nguvu ya utupu, utaratibu kwa kujaribu kumsaidia mama ajifungue ni kama ilivyo kwenye forceps. Pale mama anapopata maumivu ya kusukuma na daktari pia atakuwa anavuta kichwa cha mtoto taratibu. Kama baada ya majaribio matatu kujifungua kumeshindikana, utahitaji kufanyiwa upasuaji wa dharura kuweza kujifungua.