Mbinu za Kumbembeleza Mtoto
Haijalishi sana sababu au kwa nini mtoto analia, ila hakuna mtu anayependa kumuona mtoto wake analia. Kama mzazi mpya, lazima utakuwa unataka kufanya jambo kumsaidia.
Unaweza ukajaribu:
- Kutembea na kuongea na mtoto wako.
- Kumbembeleza na kumuimbia mtoto wako.
- Kumpeleka mtoto wako kwenye chumba chenye ukimya na chenye mwanga hafifu, kama unahisi alikuwa kwenye mwanga mkali na kelele kwa muda mrefu.
- Unaweza ukaweka sauti zinazojirudia rudia zinazofanana na sauti alizokuwa anazisikia akiwa tumboni. Sauti za kelele nyeupe (white noise sounds) zinasaidia. Mfano wa sauti hizi ni kama sauti ya maji yanamwagika toka kwenye bomba, sauti ya mapigo ya moyo n.k.
- Kumfanyia mtoto wako massage ya tumbo huweza kusaidia maumivu ya tumbo yatokanayo na kujaa gesi
- Jaribu kumnyonyesha au kumpa maziwa.
- Jaribu kumuogesha na maji ya vuguvugu.
- Mfungie mtoto wako kifuani au mgongoni kwa kanga au mbeleko maalum ya kubebea watoto, na uzunguke zunguke nae nyumbani kwako
- Toka nje na mtoto wako kama hali ya hewa inaruhusu. Mabadiliko ya mazingira na kupata hewa safi inaweza ikasaidia
- Unaweza ukamuweka mtoto wako kwenye kigari chake na mkaenda kutembea tembea
- Jaribu kuweka muziki unaojua mtoto wako anapenda
- Muweke mtoto wako kwenye kibembea chake kama unacho na ukisukume mbele na nyuma taratibu ukipunguza nguvu kadiri unavyomuona analala.
Kama unavyoona, kuna mbinu mbali mbali unaweza kutumia kumbembeleza mtoto wako. Ila mbinu hizi sio zote na haimaanishi kwamba mbinu hizi ni suluhisho kwa kila mtoto. Kumbuka kwamba watoto wote ni tofauti. Jitahidi kujua mbinu zipi zinaweza kukusaidia kwa mtoto wako. Ila usishangae, njia inayokusaidia kumbembeleza mtoto wako wiki hii, isikusaidie wiki 2 zijazo. Ila ni sawa pia kwani wakati mwingine watoto huamua kulia tuu.